Jina lake
kamili ni John Patrick Amama Mbabazi, lakini hujuilikana zaidi kama
Amama Mbabazi. Alizaliwa Januari 16, mwaka 1949 kwenye kijiji cha Mparo
katika kaunti ya Rukiga, iliyoko katika wilaya ya sasa ya Kabale.
Mbabazi
alisoma katika taasisi mbili maarufu nchini Uganda wakati wa kipindi cha
ukoloni na baada ya ukoloni- Chuo cha Kigezi kilichoko Butobere ambako
alisomea masomo yake ya sekondari, na kisha shule ya Ntare alikosemea
masomo ya juu ya sekondari. Mbabazi ana Shahada ya Kwanza ya Sheria
aliyoipata kwenye Chuo Kikuu cha Makerere.
Mwaka
1976 alipata diploma ya uzamili ya Sheria kutoka kituo Chuo cha
Maendeleo ya Sheria mjini Kampala. Mbabazi ni wakili wa Mahakama za
Uganda na tangu mwaka 1977 amekuwa mwanachama wa chama cha wanasheria wa
Uganda.
Taaluma, kazi na siasa
Kabla ya
kujiunga na siasa, alifanya kazi kama wakili wa taifa katika ofisi ya
Mwansheria Mkuu kuanzia mwaka 1976 hadi 1978, na kisha kupanda cheo na
kuwa katibu wa Baraza la Sheria la Uganda kuanzia mwaka 1977 hadi 1979.
Amama Mbabazi na Yoweri Museveni, marafiki wa zamani waliogeuka wapinzani wa kisiasa.(VICTOR)
Kati ya
mwaka 1986 na 1992, alifanya kazi kama mkuu wa Shirika la Usalama wa
ndani. Pia alikuwa Waziri wa nchi katika Ofisi ya Rais, anayeshughulikia
masuala ya siasa. Kati ya mwaka 1986 na 1992, alikuwa naibu waziri wa
Ulinzi. Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Waziri wa Ushirikiano wa Kikanda
kuanzia mwaka 1998 hadi 2001. Mwaka 2004, aliteuliwa kuwa Mwanasheria
Mkuu wa serikali na Waziri wa Sheria.
Mbabazi
alishikilia wadhifa huo hadi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi mwaka
2006, nafasi aliyoishikilia hadi alipoteuliwa kuwa Waziri wa Usalama,
kuanzia Februari mwaka 2009 hadi Mei 2011, wakati alipoteuliwa kuwa
Waziri Mkuu wa Uganda.
Alikuwa
katibu wa kundi la wawakilishi wa NRM katika Bunge la Katiba ambalo
liliandaa Katiba ya Uganda mwaka 1995, na alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu
wa chama cha National Resistance Movement (NRM) kuanzia Novemba mwaka
2005 hadi Januari, 2015.
Waziri Mkuu chini ya Museveni
Mbabazi
ni waziri mkuu wa 10 katika historia ya Uganda na alitoa mchango muhimu
katika harakati za ukombozi za Uganda kutoka tawala za kidhalimu kuanzia
mwaka 1972 hadi 1986 na ni mwanachama mwanzilishi wa chama tawala cha
NRM.
Waziri Mkuu wa zamani wa Uganda, Amama Mbabazi, akizungumza na vyombo vya habari mjini Jinja.
Mbabazi amekuwa mbunge wa jimbo la Kinkiizi Magharibi katika wilaya ya Kanungu, nafasi aliyoishikilia tangu mwaka 1996.
Rafiki wa
utotoni wa Mbabazi, Ruhakana Rugunda aliteuliwa na Rais wa Uganda,
Yoweri Museveni, kushika nafasi ya Mbabazi kama Waziri Mkuu, Septemba
18, mwaka 2014. Hatua hiyo ilionekana na wengi kama njia ya Rais
Museveni kumuadhibu Mbabazi baada ya kuwepo uvumi kuwa anataka kugombea
urais.
Juni 15
mwaka 2015 Mbabazi alitangaza nia yake ya kuwania nafasi ya kuteuliwa
kugombea urais dhidi ya Rais Museveni ndani ya chama cha NRM, wakati wa
mkutano wa chama hicho Oktoba 4 mwaka 2015.
Julai 31,
baada ya kuwepo kutoelewana na kutokubaliana kwa kiasi kikubwa kati ya
maafisa waandamizi wa chama hicho na Mbabazi mwenyewe, waziri huyo mkuu
wa zamani wa Uganda alitangaza kuwa atasimama kama mgombea binafsi.
Tangazo hilo lilijibiwa na Rais Museveni, alielitaja kama "mwenendo
mbaya ulioonyeshwa mapema na Mbabazi."
Mbabazi
anaungwa mkono na muungano wa Democratic Alliance unaojumuisha vyama
kadhaa vya upinzani nchini Uganda, pamoja na makundi ya wanaharakati na
watu mashuhuri.
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269