Breaking News

Your Ad Spot

Nov 21, 2015

PAPA WEMBA ; MKONGO MKONGWE ASIYECHUJA SAUTI

PAPA WEMBA
UKITAJA wakongwe na wakali wa sauti barani Afrika usipomtaja mwanamuziki wa dansi kutoka Kongo, Jules Shungu Wembadio Pene Kikumba ‘Papa Wemba’, utakuwa umekosea sana!
Wemba ni mkongwe katika sanaa na muziki lakini sauti yake tamu na nzuri bado iko vilevile licha ya umri kuonekana umemtupa mkono.
HISTORIA YAKE
Alizaliwa mwaka 1949 katika eneo la Lubefu mkoani Sankuru katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
MUZIKI WAKE UNA MAJINA KIBAO
Ni mwanamuziki wa miondoko ya Lese- Rhumba ambayo baadaye ilijulikana kama Soukous, Afro Pop Soukous, African Traditions na Central African.
NYIMBO ALIZOIMBA
Zipo nyimbo na albamu nyingi alizofanya miongoni mwao ni pamoja na Pauline alioufanya mwaka 1970 akiwa na Kundi la Zaiko Langa Langa mwaka 1995 aliachia albamu ya Emotion ikiwa na wimbo mkali wa Show Me The Way, mwaka 1996 alifanya Wimbo wa Wake-Up 1996 akishirikiana na Koffi Olomide, mwaka 2014 aliachia albamu ya Maître D’école-Teacher.
Nyingine ni Esclave, Maria Valencia, Lingo Lingo, Madilamba na Mwasi.
UMAARUFU WAKE
Wemba ni mwanamuziki maarufu sana barani afrika na hata duniani. Anatajwa kama mmoja wa wasanii wa kwanza walioanzisha Bendi ya Soukous Zaiko Langa Langa mwaka 1969 mjini Kinshasa akiwa na wanamuziki kama Nyoka Longo Jossart, Manuaku, Pepe Felly, Evoloko na wengineo.
Mwaka 1977 alianzisha Bendi ya Viva la Musica akiwa na vijana wenye vipaji kutoka kijijini kwao na kufanikiwa kuachia nyimbo kama Mere Superieure, Mabele Mokonzi, Bokulaka na zinginezo.
NI MUIGIZAJI
Mbali na uimbaji, Wemba pia ni muigizaji na alishawahi kushiriki katika filamu ya La Vie Est Belle- Maisha ni Bora iliyofanikiwa sana nchini Zaire (Kongo kwa sasa) mwaka 1987.
SKENDO
Mwaka 2003 alishukiwa kuhusika katika mtandao ambao inadaiwa walivusha mamia ya wahamiaji haramu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (zamani Zaire) hadi Ulaya, Papa Wemba alikamatwa nyumbani kwake mjini Paris na kufungwa jela miezi mitatu na nusu na baadaye kuachiwa baada ya kutokupatikana na hatia, ndani ya mwaka huo aliachia albamu ya Somo Trop ikiwa na wimbo unaozungumzia kile kilichomkuta maishani mwake.
HIVI KARIBUNI
Mkali huyo wa sauti, hivi karibuni alitua Bongo kwenye Tamasha la KARIBU MUSIC FESTIVALS 2015 lililofanyika Novemba 6, Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani na kuacha historia ya aina yake kutokana na kutozeeka sauti na kuonesha umahiri wa hali ya juu katika uimbaji.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages