Breaking News

Your Ad Spot

Jul 28, 2015

BALOZI MULA MULA AAGA RASMI WATANZANIA WAISHIO MAREKANI

Na Mwandishi  Maalum
Katibu Mkuu, Wizara ya  Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,   Balozi Liberata Mulamula (Pichani), amewaaga watanzania waishio nchini  Marekani,  kwa kuwataka kujivunia utanzania wao na kutoionea aibu lugha yao ya taifa,   Kiswahili.

Mwishoni mwa wiki,   Ubalozi wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania nchini Marekani,  uliandaa hafla ya aina yake  ya  kumpongeza, kumshukuru na kumuaga  Balozi Liberata  Mulamula ambaye sasa ni  Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.


Hafla hiyo iliyowajumuisha  watanzania wa kada mbalimbali wakiwamo maafisa na  wafanyakazi wa Uwakilishi wa Kudumu wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, wakiongozwa na   Balozi  Ramadhan  Mwinyi,  ilipambazwa kwa nasaha mbalimbali na salamu za kumtakia kheri Balozi Mulamula katika  jukumu lake jipya.


Pamoja na  kusikiliza salamu kutoka kwa wawakilishi  wa makundi ya  kijamii,  na  kupokea zawadi,   Katibu Mkuu, Balozi Mulamula naye alipata fursa ya  kuzungumza mawili  matatu.


Katika  salamu zake  kwa watanzania  waliojumuika katika makazi yake.  Moja ya mambo muhimu  aliyoyazungumza ni pamoja na kuwaasa  watanzania waishio nchini   Marekani, kujivunia utanzania wao,  umoja wao na kubwa zaidi kutoona aibu kuizungumza na kuiendeleza lugha ya taifa Kiswahili.


“Niwaombeni  jambo moja,  msione aibu kuzungumza lugha yetu, lugha yenu ya Kiswahili,  miaka kadhaa iliyopita  watanzania waughaibuni walikuwa hawazungumzi  Kiswahili , waliogopa kujitambulisha kwa lugha yao,  lakini sasa hali imebadirika sana,  unakutana na watanzania kila kona wanazungumza Kiswahili   hili ni jambo la kujivunia sana na ninawaomba   tuendeleze utamaduni huu wa kuzungumza Kiswahili, kuwa ugenini hakumaainishi  uachane na  lugha yako” akasisitiza Balozi Mulamula na kushangiliwa na watanzania.


Katika  kutilia mkazo  wa lugha ya  Kiswahili,   Balozi  Mulamula aliwataka wana DMV kuendelea na darasa la kuwafundisha watoto  lugha hiyo ya Kiswahili na  maeneo mengine kuiga mfano huo.


Jambo  jingine ambalo Balozi  alililowasisitizia watanzania  hao ni kuhusu upendo, mshikamano, kuheshimiana, kusaidia na kutobaguana kwa misingi ya dini, kabila,  eneo  ambalo mtu  anatoka au kwa misingi ya itikadi za kisiasa.


“ Ninaondoka  baada ya miaka miwili ya kuwa   Balozi wenu,  na katika miaka hii miwili nimejifunza mengi sana kutoka kwenu, mmeshirikiana nami  na Ubalozi katika mambo mengi yakiwamo ya kuchangia maendeleo yenu wenyewe na maendeleo ya watanzania wenzenu endeleeni na moyo huu”.


Kaongeza “nitakuwa nanyi na kama  mjuavyo  tunakitengo kizima kinachoshughulia masuala ya diaspora, na kama ningekuwa mwanasiasa basi  nyie wanadiaspora mngekuwa  mtaji wangu,  jimbo langu”. akabainisha na kuamsha tena   vifijo kutoka kwa wana-diaspora hao.


Katika hatua nyingine,   Katibu Mkuu, Balozi Mulamula amewahimiza  watanzania walioko nje, kumchangamkia   hasa kwa wale wenyekutaka kujaza fomu za maombi ya pasi zao za kusafiria ambazo zimekwisha muda.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages