Breaking News

Your Ad Spot

Mar 30, 2015

JENERALI MWAMUNYANGE: MAMLAKA ZA MISHENI ZA ULINZI WA AMANI ZIWE WAZI

Na Mwandishi Maalum, New York
Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, amelishauri   Baraza Kuu la  Usalama la Umoja wa Mataifa,   kuweka  bayana    na kwa uwazi mamlaka ( mandate) ambayo misheni ya kulinda Amani itapaswa kutelekeza  kule inakopangiwa kwenda.

Ametoa  ushauri huu   siku ya Alhamisi  wakati alipokuwa akitoa mchango wake kwenye mkutano wa Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi  ambao nchi zao zinachangia  katika operesheni za ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa.

Katika  mkutano huo uliokuwa wa siku moja, na kuhudhuriwa na  Wakuu wa Majeshi  na  Maafisa wa Ngazi za Juu ,kutoka nchi 108, Jenerali  Mwamunyage amesema;
“ Wakati wa utoaji wa idhini na mamlaka kwa   misheni ya   kulinda Amani,  Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,  linatakiwa kumwita mbwa kwa  jina lake kama lilivyo.Mbwa aitwe kwa jina lake. Elezeni bayana na  kwa    uwazi  mamlaka na idhini  za utekelezaji za ya misheni ”

Na kuongeza, “ iwekwe wazi, kama ni misheni ya kulinda Amani, basi ielezwe ni ya kulinda Amani, na kama  ni  ya matumizi ya nguvu  basi na iwe hivyo”. Amesisitiza Mkuu wa Majeshi
Amesema kwamba, kwa kutamka  jina halisi /mamlaka  ya misheni  pale inapoundwa,  Baraza Kuu la Usalama  linakuwa linapeleka ujumbe ulio sahihi kwa pande zote zinazohusika  pamoja na nini wakitarajie.

Jenerali Mwamunyage ameuleza washiriki wa mkutano huo  mkutano wa kwanza wa aina yake  kuwakutanisha Wakuu wa Majeshi zaidi ya mia moja, wakati mmoja na mahali pamoja. Kwamba, uwazi huo pia utasaidia  kuweka bayana hatua za utekelezaji  zinazofanywa  na walinzi wa amani   kwenye eneo la utekelezaji.

Vile vile Mkuu wa Majeshi ya Tanzania ameshauri pia kuwa misheni  ambayo tangu  kuundwa kwake zilikuwa na mamlaka ya kutumia nguvu,   ni vema zisiendelee kutambuliwa hivyo pale mamlaka ya misheni hiyo  yanapobadilika  kutoka matumizi ya nguvu na kuwa misheni ya kulinda Amani au jina lolote lile.

Tanzania  inawanajeshi wake katika Misheni mbalimbali  ikiwa ni pamoja na   UNAMID ( Darfur) UNFIL, ( Lebanon) MONUSCO ( DRC) na katika maeneo mengine. Vile vile Tanzania ina Polisi na  Askari Magereza ambao nao wanahudumu katika misheni mbalimbali.

Akizungumzia kuhusu mkutano huo ambao ulifunguliwa na  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na  Ban Ki Moon na kufungwa na  Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson.  Jenerali Davis Mwamunyange amesema,  mkutano kama huo unapashwa kuitishwa mara kwa mara kwa kuwa unawawezesha  wakuu wa majeshi kubadilishana uzoefu wao katika utekelezaji wa  operesheni za ulinzi wa Amani na hasa kwa kuzingatia kwamba nchi wanachama ndio wanaotoa wanajeshi wao na ndio  haswa wanaokumbana na changamoto mbalimbmali za utekelezaji wa  dhamana hiyo.

Awali akifungua mkutano huo,   Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon  pamoja na kuwashukuru  Wakuu hao wa Majeshi kwa mchango wao katika eneo hilo la  ulinzi wa Amani,  amesema   operesheni  ya kulinda Amani chini ya Umoja wa Mataifa,  licha kwa kwamba ni  dhamana inayohitajika sana  lakini pia inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Akazitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa  ni  upugufu wa raslimali fedha,  zana,  vifaa na teknolojia za kisasa lakini pia ugumu na hatari wanazokumbana nazo walinzi wa Amani, ambapo  hivi sasa mbinu za kigaidi na uvamizi kwa walinzi wa Amani ni baadhi ya changamoto na hatari wanazokumbana nazo.

Katibu Mkuu, amewataka wakuu hao wa majeshi kuongeza ushirikiano wao kwa  Umoja wa Mataifa na hasa katika kutafuta mbinu za kukabiliana na changamoto za kiulinzi na kiusalama ambazo duni hivi sasa inakabiliana nao.

Akaongeza kuwa   kujitokeza kwa idadi kubwa ya wakuu hao wa majeshi ya  ulinzi kushiriki mkutano  huo, kumeipa faraja kubwa  Umoja wa Mataifa.

Naye  Naibu Katibu Mkuu Jan Eliasson, akihitimisha mkutano huo, amewataka wakuu hao wa majeshi na serikali zao kuendelea na majadiliano  ya mchakaTo wa  kuundwa kwa majeshi ya ulinzi ya kikanda,  majadiliano ambayo  yanatakiwa kuendelea  kuelekea mkutano wa Operesheni ya Ulinzi wa Amani  utakaofanyika mwezi  Septemba mwaka huu.

     Wakuu hao wa Majeshi ya Ulinzi pamoja na kutoa mchango wa mawazo yao, pia walipata fursa ya kupata maelezo kutoka kwa  Viongozi wakuu waandamizi wanaoongoza    Idara zinazozohusu  Operesheni ya Ulinzi wa Amani.

-------------------------------------------------------
HABARI KATIKA PICHA
 " Mnatuwakilisha vema?" ndilo swali ambalo   Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,  Jenerali Mwamunyange alilowauliza watanzania hawa wawili,  Afisa wa Usalama wa UN Bw. Jacob Mwashiozya na  Bw.  Joseph Msami, wa Idhaa ya Kiswahili  ya Umoja wa Mataifa walipokuwa  wakisalimiana naye na ujumbe wake  mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa wakuu wa majeshi ya ulinzi
 Jenerali Davis Mwamunyange (watatu kushoto), akiwa na ujumbe wake mbele ya bendera ya Tanzania, baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku moja wa Wakuu wa Majeshi ya  Ulinzi kutoka nchi 108. Kutoka kushoto ni  Kanali Adolf Mutta, Brigedia Jenerali Luwogo, Brigedia Jenerali Kamunde,  Meja Ngh'abi, na  Luten  Kanal Itang'are
  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akiingia kwa staii ya aina yake wakati alipokwenda kufungua mkutano wa kwanza wa aina yake  kufanyika  katika Umoja wa Mataifa,  ambapo Wakuu wa Majeshi  ya ulinzi kutoka  nchi zaidi ya 100 walikutana kwa wakati mmoja na mahali pamoja kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu operesheni za ulinzi wa amani za umoja wa mataifa.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni kistaarab kwa Hoja kwa faida ya wenzako. au tundikie kupitia nkoromo@gmail.com, simu 0672223269

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages